Thursday, April 27, 2017

Zifahamu Dalili kuwa Ndoto zako zinakwenda Kufanikiwa

Kwa kawaida kila Mwanadamu huwa na matarajio ya namna anavyoweza kutimiza malengo yake,hizi zinaitwa ndoto. Ndoto ni maono ya siku zijazo ambazo Mwanadamu anategemea zitakuwa kweli na zitadhirika katika ulimwengu unaoonekana. Ndoto hizi au maono yako,zimegawanyika katika makundi mawili ambazo ni; Long term dreams\long term plan,haya ni malengo ya mda mrefu ambayo mwanadamu anajiwekea,kwa mfano,ulishawahi kukaa na mtoto mdogo ukamuuliza baadae alikuwa angependa kuwa nani??wengine wanasema wanapenda kuwa madaktari,wengine wanapenda kuwa Maaskari,kila mtoto na malengo yake,hizi huitwa ndoto za mda mrefu,itachukua miaka mingi kuziona zikitumia. Aina ya pili ni shirt plan dream\shirt plan,hii ni mipango ya mda mfupi,ambayo mtu amejipangia,mfano ushawahi kuona mfanyakazi anajipangia kufanya kazi kwa bidii ili aje kuwa mfanyakazi bora,aina hii ya ndoto huitaji maandalizi ya mda mfupi kutimia. Sasa ili ndoto yako itumie,vipo vichocheo vinavyofanya ndoto itimie,naanza kuvitaja ili ulifahamu. 1.Ndoto inayokwenda kutimia ni lazima ipingwe: Hii ni sifa kuu ya kwanza ya ndoto inayokwenda kutimia,utashangaa baada ya kuwaeleza watu ndoto yako,wapo watakaoipinga,mfano unakuta mtu ana kipato kidogo lakini ana mpango wa kufungua kampuni kubwa,sio kama uwezo hana wala vigezo hana,hapana,lakini wataibuka watu wa kumuambia hauwezi,japo ipo mifano mingi ya waliofanikiwa wakiwa na mitaji midogo au pengine hawakuwa na mitaji kabisa,kwa sababu tu,watu wanaolizunguka wameshaona wao hawakufanikiwa walipojaribu unachotaka kuliharibu,hivyo watakupinga. 2 Ni lazima ndoto yako itapata wafuasi: Hawa ni wale watu watakaokutia moyo kuwa usiogope,wapo waliofanikiwa,wewe ni nani ushindwe,hawa watakutia nguvu na kukushauri pale unapokwama,wengi watakuweka karibu na kupenda kujua kupanda na kushuka kwako,changamoto unazopitia na watakuwa karibu nyakati zote. 3 Utasalitiwa: Fahamu sio wote wanaokuja kwako na kukuambia tupo pamoja katika safari yako,hivyo wapo wapo wengine watakaokusaliti,ipo mifano mingi ya usaliti,biblia inawataja akina Yuda,utakaponiona hili usiogope,fahamu ndoto yako ina nguvu na ina uwezo mkubwa wa kufanikiwa. 4 Itakugharimu: Ndoto inahitaji maandalizi na mipangilio,tegemea kutoa sadaka mda wako ili kutafuta uwezekano,utautumia mda wako kusoma waliofanikiwa katika eneo la ndoto zako,kama wewe unapenda siasa na haukubaliki,utajikuta kuna mda unatenga kusoma mbinu walizotumia watu wasiokubalika na wakashindwa,kama wewe ni mwanauchumi pia itajitahidi kujua waliofanikiwa wakiwa na kipato cha chini na wakafanikiwa,mda mwingine maandalizi ya gharama hugharimu pesa na vitu kama resources nyingine za kuifanya ndoto zako ziwe kweli. 5 Utapoteza Marafiki: Unapotimiza ndoto zako kuna baadhi ya marafiki utawapoteza hasa wale watakaoingia katika kundi la kukupinga,kwa mfano unatamani kuwa mfanya biashara mkubwa,tegemea kuna marafiki ambao ulikuwa unatumia mda nao katika mambo mengine wataona amebadirika,hivyo watajiondoa wenyewe. Mda mwingine inabidi ili uwe mtu wa ndoto flani flani,kuna makundi ya watu itabidi uachane nao ili kutengeneza sifa itakayokuletea ustawi,mfano huwezi kuwa na ndoto ya kuwa Mbunge au Rais wa taasisi iwapo ulio nao wanahakisi sifa zitakazokufanya watu wasiuamini,lazima uwakwepe na uanze kutafuta marafiki wapya wanaoendana na sifa ya ndoto zako. 6 Nitakuletea Connection ya watu: Moja ya ndoto inayokwenda kutimia,utaanza kukutana na watu usiowategemea,ndoto inayokwenda kutimia huwa na tabia ya kukuunganisha na watu tofauti tofauti kwa urahisi zaidi,kwa mfano unatamani kuwa mwanasiasa mzuri,utashangaa unaanza kuwa na marafiki wengi wanasiasa ambao wana mafanikio nao wataanza kuzisikia habari zako,utashangaa wanaanza kuja siku hadi siku tunafahamiana na watu wengi ambao hukuwahi kufikiria,au unatamani kuwa mwanauchumi mzuri,utashangaa inakutana na watu waliofanikiwa hilo eneo na mnakuwa marafiki kwa mda mfupi,ukikiona hilo fahamu hiyo ndoto yako inakwenda kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. 7 Ndoto itajitangaza yenyewe: Ndoto huwa haijifichi,utashangaa watu wanaanza kujua hata bila ya kukitambulisha wewe ni nani kutokana na tunavyoongea,watu watajua ndani yako una ndoto kubwa,kwa mfano,mara nyingi watu wengi huniambia "wewe unafaa kuwa mwanasiasa" kwa nini,kwa sababu ya namna ninavyoongea na jinsi ninavyodadavua mambo,mwingine anakuuliza "una mpango wa kugombea popote?" na sio kweli kuwa ulijitangaza wewe ni mwanasiasa!!ni wao tu kwa kukusudia,wakajua ni nini unacho ndani,au mara nyingi unakuta mtu anakufananaisha na mtu fulani aliyefanikiwa moja kwa moja kutokana na misimamo yako,sio kama ulimwambia laa hasha kwa sababu ndoto huwa na tabia ya kujitangaza yenyewe. 8 Utakutana na mazingira yanayoipinga ndoto yako: Hii ni dalili nyingine kuwa unaenda kufanikiwa,mambo yatakuwa magumu na mazingira ya kutimia ndoto yako yatakuwa magumu mno,hii ni kwa sababu ndoto ni kitu cha thamani,huwa kinapiganiwa ili akitumie,Fuatilia historia ya Baracj Obama,japo alikutana na ugumu wa maisha na alitoka katika familia ambayo huwezi kufikiria itatoa Rais wa Dunia lakini alikuwa na ndoto hiyo mda mrefu licha ya umasikini aliokuwa nao hapo hawali na ili uwe Rais wa nchi kubwa kama Marekani ni lazima uwe umejitosheleza kichumi. Ukijitazama na kuitazama namna ndoto yako ilivyokuwa kubwa na mazingira unayekutana nayo ni tofauti,ujue hiyo ni ndoto inayokwenda kutimia punde. 9 Italeta ushindani: Unaweza ukafikiria upo peke yako unayetafuta nafasi ya kutimiza malengo yako,lakini yupi mwingine nae anawaza kama wewe,kutumia fursa hizo hizo ulizowaza kuzitumia,inapokuja kwenye kutimiza malengo mnakutana,hapo ndipo huja "kivumbi na Jasho" hadi mwenye nguvu na akili kumzidi mwenzake ashinde,kwa kifupi,ndoto inayokwenda kutimia huwa na ushindani mkubwa tofauti na ndoto zisizo kwenda kutimia. 10 Ndoto huweza ikachelewa kutimia,hii ni sifa ya msingi,sio mara zote wengi huweza kwenda moja kwa moja kwenye kutimiza ndoto zao,wengine huchukua mda,wakaanguka na kuinuka tena,unapoona unashindwa kutimiza ndoto yako lakini ndani kunadai uendelee maana yake mda bado,unahitaji tujifunze zaidi na zaidi bila kuchoka,weka juhudi,fahamu nini kilikukwamisha alafu jaribu tena pasipo na kuchoka,sio wote wanapofanikiwa moja kwa moja na tunayo mifano. Kwa kifupi,ndoto hupiganiwa,ndoto huchochewa ili ikue na kutimia,wengi walijaribu,hawakufanikiwa wakajaribu tena na tena,amini wewe ndio mwenye ufunguo wa hizo ndoto zako,usiruhusu mazingira au watu wakutoe kwenye ramani,jifunze kila siku changamoto zipo na lazima ukabiriane nazo!! Usikate tamaa!

Sunday, April 20, 2014

Usome waraka wa maaskofu Bunge la katiba huu hapa

“Sote tuwe na Umoja” (rej. Yn 17:21) UTANGULIZI wapendwa, tunapohitimisha kipindi cha Kwaresima kilichokuwa na ujumbe: “Ukweli utawaweka huru” (Yn. 8: 32), tunawaletea ujumbe wa “Umoja” ili kuongeza msisitizo kwenye ujumbe wetu wa Kwaresma. Tunaitwa kukubali kuwa umoja ni ukweli msingi wa kila mafanikio ya jumuiya ya mwanadamu. Ufufuko ni Pasaka inayomaanisha kivuko au kupita kwa Wayahudi toka kwenye matatizo ya utumwa hadi uhuru kamili. Kwa Wakristo ni kuvuka kutoka utumwa wa fikra za kifo (dhambi) hadi uhuru kamili wa ufufuko wetu na Bwana Yesu. Kwahiyo, furaha za Pasaka zinapaswa kusheheni shukurani za dhati kwa zawadi nyingi alizotujalia Mungu Muumba wetu tokea mwanzo na hasa nyakati hizi katika mwanga wa Ufufuko wa Kristo. Adhimisho la Pasaka litawaliwe na furaha, amani na matumaini makuu yaliyoletwa kwa Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Mtume Paulo anatuambia: “Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo” (1Kor. 15:57). Wakati dhambi na kifo husababisha kujitenga; uhuru, furaha na amani husababisha kuungana. Ndivyo ilivyotokea kwa Adamu na Eva. Walipokuwa bila dhambi walikuwa huru, wenye furaha, amani na umoja na Mungu. Walipotenda dhambi walimkimbia Mungu, wakatafuta kujificha. Hata wao wenyewe walioneana aibu na hatimaye wakafukuzwa kutoka kwenye bustani ya Edeni (Mwa. 2:25; 3:7-8, 23-24). 1.Ndugu zetu katika Kristo, “Amani iwe Kwenu” (Yn. 20:19). Wakati huu wa Pasaka, wakati ambao pia mchakato wa kuandika Katiba ya nchi yetu unaendelea, hatuwezi kuacha kutafakari kwa dhati juu ya umoja wetu sisi Watanzania. Bila shaka, moja ya mihimili mikubwa ya umoja wa kitaifa ni uongozi bora. Mwenyezi Mungu aliwatoa watu wake utumwani Misri na kuwaweka huru kwa kuwateulia viongozi miongoni mwao. Kiongozi wa kwanza alikuwa Musa (Kut. 3:10). • Chini ya uongozi wa Musa Wayahudi walichukua muda mrefu kujenga umoja na uelewa, kwamba walikuwa watu wa Mungu na walipaswa kumtambua kiongozi wao kama mteule wa Mungu (Kut. 16:3; 17:4. • Katika kutangatanga kwao jangwani, iliwachukua pia muda mrefu kutambua uovu wao na kujitakasa dhidi ya dhambi zao (Kut. 32:1-14). • Hata wakiwa tayari katika nchi waliyoahidiwa hawakuacha machukizo yao kwa Mungu pamoja na kukanywa mara kwa mara na Manabii wake Mwenyezi Mungu (Amu. 2:11-13). Wakati ulipowadia, Mungu alimtuma Mwanae Yesu Kristo kujenga Utawala wa Mungu juu ya msingi wa imani na ukweli (Gal. 4:4): • Imani kwa Mungu na imani baina ya watu wenyewe – kuaminiana – ndio msingi wa Utawala wa Mungu (2Thes. 2:13-17). • Lakini kutokana na udhaifu wa kibinadamu, mara nyingi tunavunja umoja wetu na Mungu na kati yetu wenyewe kwa kiwango cha kutotaka kuishi pamoja; tunabaguana na hatutendeani haki (Mwa. 4:7-8). Katika ulimwengu wa leo, tunashuhudia madhara ya utengano wa namna nyingi. Dhambi nyingi za binadamu zinasababisha mifarakano na vita. Hayo ni matukio ya kila mara katika nchi nyingi ulimwenguni na hasa kwetu Afrika. Hata historia yetu wenyewe ina matukio mengi ya jamii kufarakana na kujizamisha katika vita. • Mababu zetu walipitia maisha marefu ya kuhamahama na kuchukuliwa utumwani na wengine kubaki watwana na watawaliwa wa kikoloni kwa vipindi virefu kabla ya kujipatia uhuru wa kujitawala. • Tulipopata uhuru, tulijifunza kujenga umoja katika tofauti zetu kubwa za kikabila na kufikia taifa moja. • Tulichukua hatua kubwa kuunganisha nchi mbili huru, Tanganyika na Zanzibar, na kuifanya kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa kielelezo kwa Bara la Afrika cha kujenga umoja. 2.Hatua zote hizo tulizopitia na tulizochukua kwa makusudi kabisa, tulikuwa na nia na utashi wa kuwa wamoja. Tulitaka kujenga maendeleo ya pamoja na mafanikio ya kila Mtanzania kufikia maisha bora. Jitihada hizi njema zimekuwepo kwa miaka hamsini iliyopita. Tumefanikisha mambo mengi katika umoja wetu ambao unatusukuma kumshukuru Mungu. Kwa muda mrefu umoja wa Watanzania umeonekana kwa mataifa mengine kuwa ni kielelezo cha umoja wa kitaifa wa hali ya juu sana. Ni umoja uliokua kufikia kiasi cha kufuta tofauti za awali za mataifa yaliyohusika kuunda umoja. Tunamshukru mwenyezi Mungu kwa kuifanya Nchi yetu kuwa kimbilio la waliokata tamaa. Tanzania imewapa wakimbizi mahali salama pa kuishi pamoja na Watanzania. Chini ya Jamhuhuri ya Muungano wa Tanzania, waliokuwa bado chini ya wakoloni, waliandaliwa kujikomboa na kuwa mataifa huru. Pamoja na mafanikio hayo makubwa, zimejitokeza dosari kadhaa katika umoja zilizofanya umoja wetu upoteze baadhi ya sifa zake za awali. Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndio ukweli. Baadhi ya Watanzania wanafikiri kuwa umoja unaofuta tofauti haufai ila umoja unaosisitiza tofauti kama ulivyo umoja wa kikanda (kama ilivyo SADC, ECOWAS, n.k) ndio unafaa! Wakati mataifa mengine yanatamani umoja unaofanana na ule umoja wetu wa awali, baadhi yetu tunatamani kurudi nyuma kwenye umoja wa mpito! Kutokana na mapungufu yaliyodhihirika ndani ya mafanikio yetu, umuhimu wa kufanya marekebisho ulidhihirika. Ni kwa sababu hiyo, watu wengi walitaka na wanataka mabadiliko au mageuzi ya msingi sana. Kwa msukumo huo ndio sababu tuliingia katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya. 3.Kazi ya kuandika Katiba si nyepesi na yataka umakini mkubwa. Haishangazi sana tunapojionea mivutano na migongano ya hoja kutoka kwa makundi kinzani katika nchi moja. Mawazo ya wengi yamewasilishwa kisheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kujadaliwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK). Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu kushinikiza kuingizwa matakwa yake kwenye Katiba kwa njia zozote zile ili kujihakikishia kuendelea kulinda maslahi yake ya kisiasa. Wajumbe wa Bunge Maalum Katiba wanazozana, wanakashifiana,wanatukanana na hawataki kuachana na itikadi za kisiasa ili kufikia muafaka katika masuala muhimu yatakayowahakikishia raia wa kawaida kushiriki kwenye fursa za maendeleo kwa manufaa ya wote. Hayo lakini yasitukatishe tamaa na kujiona kama tu watu wa kushindwa wakati tukiwa bado kwenye mchakato mrefu wa kujipatia jukwaa jipya kwa mustakabali wa taifa letu Tanzania. Tushirikiane na wote wenye nia njema kupambana na nguvu za maovu na ubinafsi na kuachana na itikadi za kisiasa na matakwa ya kiuchumi ya matabaka ya walio nacho ili kupigania haki za wanyonge. Tuandae Katiba ambayo itatupatia misingi imara ya maadili itakayotuongoza kupigana dhidi ya ubinafsi na ufisadi, na kutetea haki za binadamu kwa wote. Vigezo vyote muhimu kwa maisha ya mshikamano kitaifa vimeandikwa katika Rasimu ya Katiba Sura ya 1 hadi ya 5. Tukisha kukubaliana na yaliyomo katika sura hizo, muundo wowote wa Serikali unawezekana kwa kuzingatia kanuni za uwiano wa madaraka na wajibu wa mihimili mitatu ya Dola kwa mujibu wa Sura za 8 hadi 15. Ili tufikie lengo letu la kuwa na Katiba bora katika hatua tuliyofikia ya mchakato wa Katiba Mpya yatubidi kuzingatia yafuatayo: • Kuheshimu kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuitumia kama ilivyokusudiwa na sheria iliyoiweka. • Kuwa na nia njema ya kweli ya kutafuta suluhisho la matatizo mengi ya utendaji katika Dola zilizopo katika Muungano. • Kuwa na hamu ya kujitoa kwa taifa na kulitumikia kwa moyo bila kutawaliwa na ubinafsi au kujipendelea kiinchi na kiukanda kwa madhumuni ya kuboresha maisha ya Watanzania wote. • Chaguo la muundo wa Dola, sharti liongozwe na malengo na madhumuni ya umoja wetu wa kutaka tuishi kwa mshikamano wa dhati. Uchaguzi wa muuungano wa serikali moja, mbili au tatu sharti ufanywe kwa dhamiri safi iliyo na uelewa uliochambua matatizo yaliyopo ya Muungano na kuridhia mfumo utakaosuluhisha matatizo hayo pasipo mashaka yoyote. 4.Baada ya kutafakari historia ya ukombozi wa mwanadamu kwa ufupi na hatua Watanzania tuliyofikia katika uhuru wetu wakati huu wa adhimisho la Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo mwaka 2014, tungependa kwa namna ya pekee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumvuvia Rais Jakaya M. Kikwete ujasiri wa kuamua kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kisheria katika wakati muafaka. Kwa mchakato huo wa Katiba, kupitia Tume yake Huru, Watanzania wamepata fursa ya kusema kila jambo lililowaelemea maishani na kuainisha namna wanavyotaka kujitawala. Wakati ulikuwa mwafaka kwa sababu kulikuwa na manung’uniko mengi ya ukiukwaji wa Katiba ya sasa ambayo hayakuweza kujibiwa na Serikali zilizopo. Hatua ya kuamua kuyakabili hayo kwa sheria ya Kurekebisha Katiba iliwapa wananchi fursa ya kutoa maoni yao bila mizozo na machafuko. 5.Tume ya Mabadiliko ya Katiba imewasilisha kwenye Bunge Maalum la Katiba Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni huru ya watu binafsi na makundi mbali mbali zikiwemo taasisi za dini, mamlaka za kiserikali na asasi huru za kiraia. Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalum la Katiba kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania. HITIMISHO Ndugu wapendwa, Wakati huu wa Pasaka, tuendelee kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili wajumbe wawe wazingatifu wa matakwa na matarajio ya Watanzania yalivyoainishwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba na Tume ya mabadiliko ya Katiba kwa kuheshimu maoni ya Watanzania na kuboresha maoni hayo kwa hekima na busara ili kulinda mstakabali wa Taifa letu; Tanzania yenye amani kwa ustawi wa watu wote. “Ingekuwa heri leo msikie sauti hii; msifanye migumu mioyo yenu”. (rej. Zab 95:7-8) Tuombe: Ee Bwana, katika upendo wako uwape neema watu wa taifa lako, waishio Tanzania. Katika upendo wako ujenge tena nguzo za imani, matumaini na mapendo katika mji nchi yetu. Watanzania wakiwa na imani, matumaini na mapendo ya haki utapendezwa na sadaka wakutoleazo; kila mtu akijitolea yeye mwenyewe kwako kama sadaka safi juu ya altare, pamoja na katika Kristo Mfufuka aliye katika Ekaristi. Mama Bikira Maria atuombee ili ndani yetu uzaliwe upya uaminifu unaotupa uwezo wa kutangaza kazi kuu ya Mungu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina. Amani ya Kristo Mfufuka iwe nanyi Ni sisi Maaskofu wenu: 1. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu wa Iringa 2. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Dar es Salaam 3. Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu, Arusha 4. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora/Kigoma Msimamizi 5. Mhashamu Askofu Telesphor Mkude, Morogoro 6. Mhashamu Askofu Gabriel Mmole, Mtwara 7. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Mwanza,/Shinyanga 8. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani, Lindi 9. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga 10. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge 11. Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC, Mbeya 12. Mhashamu Askofu Augustino Shao, Cssp, Zanzibar 13. Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi, Sumbawanga 14. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara 15. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba /Singida Msimamizi 16. Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba 17. Mhashamu Askofu Damian Dallu, Geita/Askofu Mkuu Mteule Songea 18. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, OSS, Kahama 19. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma, Njombe 20. Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa, Tunduru-Masasi 21. Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Mbulu 22. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma 23. Mhashamu Askofu Issac Amani, Moshi 24. Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga 25. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, Same 26. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara 27. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Dar es Salaam 28. Mhashamu Askofu Renatus Nkwande, Bunda 29. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga, Mpanda /Dodoma 30. Mhashamu Askofu Bernadin Mfumbusa, Kondoa 31. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga

Friday, November 8, 2013

HOTUBA YA RAIS KIKWETE BUNGENI TAREHE 7-11-2013





HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ALIYOITOA BUNGENI KUHUSU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, 7 NOVEMBA, 2013, DODOMA

Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;

Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.

Mheshimiwa Spika;
Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba. Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata. Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika kwa mafanikio.

Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.

Mheshimiwa Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980 ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu. Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.

Tumewaomba Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa. Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa. Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini. Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia itatuhukumu vibaya.

Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika;
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.

Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda visivyo tuseme, watawajibishwa ipasavyo.

Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika;
Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.

Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili. Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami tu. Kwa kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo.

Aina ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani ipatikane. Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo. Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.

Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi kufanya hivyo. Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu shupavu. Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema. Ameen.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.

Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao. Jambo lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.

Mheshimiwa Spika;
Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5) Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7) Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8) Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.


Mheshimiwa Spika;
Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?

Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine. Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki katika ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.

Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika kwenye masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna Lake Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo.

Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.

Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo. Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.

Mheshimiwa Spika;
Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.

Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba, 2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza? Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?



Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho. Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika;
Kwa kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke! Au sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na tutaendelea kuwepo!

Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.

Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing). Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?) Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli. Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.

Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini hivyo.

Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake hazina mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu kuliko yote Afrika.

Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.

Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu. Mimi siamini kama kuna mengine. Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri.


Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.

Mheshimiwa Spika;
Ni kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya kukamilisha baadhi ya hatua. Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara. Na, msingi huo si mwingine bali utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama wote sawia.

Mheshimiwa Spika;
Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu. Kama ngazi hizi tatu za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.



Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja. Kwa msimamo na mtazamo wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho. Na huo siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, Kamati ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.

Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake. Watanzania wengi sana wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004 iliyoongozwa na Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo. Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.

Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua. Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa miaka mitano. Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa kura. Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.

Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake. Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari.

Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.

Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake. Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi.
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza

Sunday, April 14, 2013

Tamko la CHADEMA kufuatia Video ya Rwakatare

Ndugu waandishi wa habari;
LEO tumewaita hapa ili kuwaomba mtufikishie ujumbe kwa Watanzania, kwamba nikiwa mwanasheria na mtu ambaye nimepata ujuzi wa kazi za ushushu, nimefanya uchunguzi matukio haya ya utekaji na utesaji na kugundua mambo mengi mno.

Uchunguzi huu nimeufanya kabla na baada ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wetu wa Ulinzi na Usalama, Willifred Muganyizi Lwakatare, ambaye hivi sasa anashitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kupanga ugaidi.

Nimefanya hivyo kwa kuangalia maslahi mapana ya taifa langu na chama changu. Katika uchunguzi wangu huo, nimegundua mambo mengi ikiwamo kuwapo kwa genge la watu ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaopanga mipango hii ya kishetani na kisha kuwasingizia watu wengine.

Angalieni mfano huu: Unaoitwa na polisi na Mwigulu Nchemba, “mkanda wa Lwakatare” unadaiwa uliwasilishwa jeshi la polisi Desemba mwaka jana. Lakini jeshi hilo halikumkamata yoyote wala kumhoji, hadi pale Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alipovamiwa na kuumizwa.

Aidha, Nchemba amedai kumiliki video ile Desemba mwaka jana, lakini rekodi hiyo iliwekwa kwenye mitandao ya kijamii (YouTube na Jamii Forum) baada ya kutekwa kwa Kibanda. Hapa mtu makini anaweza kujiuliza, hiki kimelenga nini?

Kwamba genge hili la kina Nchemba na wenzake, walipanga kumteka Kibanda, wakatimiza lengo lao hilo, baadaye wakaingia kwenye plani B ya kutaka kuihusisha Chadema. Wakamtumia Ludovick Joseph Rwezahula ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, kufanikisha mkakati wao huu wa kishetani.

Ndugu waandishi wa habari;
Huu ni mchezo mchafu na wahatari mno ambao kwa vyovyote vile, haupaswi kuvumiliwa. Kuanzia sasa nimeamua kwa dhati kabisa, kukomesha mchezo huu ambao unahatarisha uhai wa taifa letu.

Kwa kuanzia, kesho Jumatatu, nitaongoza jopo la mawakili sita wa Chadema kumtetea Bw. Lwakatare. Wenzangu wengine katika kesi hii, ni Profesa Abdallah Safari, Tundu Lissu, Edson Mbogoro, Peter Kibatara na Nyaronyo Kicheere. Huko mbele tutaongeza mawakili wengine, akiwamo mmoja anayewekwa na familia ya Lwakatare.

Ndugu waandishi wa habari;
Mnaweza kujiuliza, kwa nini Chadema kimechukua uamuzi huu wa kuweka kundi kubwa la wanasheria katika kesi hii ya Lwakatare? Jibu ni kwamba tumegundua kuwa kesi hii imefunguliwa kwa lengo maalum la kuidhoofisha Chadema na kuinusuru CCM ambayo inakabiliwa na dhahama ya kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na kushamiri kwa makundi.

Hivyo wameamfungulia kesi Lwakatare, kwa lengo la kutaka kuaminisha umma kuwa Chadema ni chama cha magaidi, kinapanga ugaidi na hivyo kichukiwe. Hilo ndilo lengo lao. Basi!

Ndugu waandishi wa habari;
Pili, nitakwenda mahakamani kuwasilisha ombi maalum la kuomba amri ya mahakama kuagiza makampuni ya simu za mkononi kuwasilisha mahakamani statement za simu za watu kumi (10) ili kusaidia mahakama kutenda haki na jamii kujua ukweli wa mambo haya.

Watu ambao nitaomba mahakama itoe amri ya kuletwa taarifa zao simu
na meseji (sms) ni Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa nchini (TISS), Jack Zoka, anayetumia simu Na. 255756xxxxx, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Lameck Nchemba, anayetumia simu tano zikiwamo 0754 xxxxx, 0757 xxxxx, 0714 008888 na 0787 513446 na Ludovick Joseph Rwezahula, ambaye simu zake ni,0715 927100 na 0753 927 100.

Mwingine ambaye mawasiliano yake yanahitajika, ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, anayetumia simu Na. 0754 003388, Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Mwananchi, Dennis Msaky anayetumia simu mbili, 0655 331010 na 0764 331010 na Bw. Sinbad Mwagha, ambaye ni afisa wa idara ya usalama wa taifa, anayetumia simu 0754 006355.

Wengine, ni Bw. Shaali Ali, afisa mwinge wa usalama wa taifa anayetumia simu Na. 0716990099, Saumu K. Malungu, mwenye kutumia simu 0719 541 434 na 0789 614 629, simu mbili zinazotumiwa na mtuhumiwa mkuu wa utekaji wa Dk. Steven Ulimboka, Bw. Ramadhani Abeid Igondo ikiwamo 0713 760 473, simu za Bw. Ridhiwani Kikwete ambazo ni 0754 xxxxx, 0784 566 299, simu ya Dr. Steven Ulimboka, ambayo ni 0713 0713 xxxxx, pamoja na simu zote tatu za Willifred Lwakatare, ambazo ni 0786 xxxxx, 0713 237869 na 0758 xxxxx.

Ndugu waandishi wa habari;
Mtu mwingine muhimu nitakayeomba mahakama itoe amri ya kutolewa kwa taarifa zake, ni mwandishi wa habari na mpigapicha wa magazeti ya serikali, Muhidini Issa Michuzi. Mwandani huyu wa Ikulu, ndiye aliyeandika ujumbe kwa njia ya emeili kuipongeza ofisi binafsi ya rais (OBR) na usalama wa taifa kwa kupata video ya Lwakatare.

Pongezi za Michuzi kwa TISS ndizo zinanisukuma kuiomba mahakama kuagiza kupatikana taarifa zake. Michuzi anaipongeza TISS kwa kuibua njama za wahalifu, lakini mimi ninajua TISS ikipata njama za aina hiyo haraka inapeleka ushahidi polisi, lakini huu wa Lwakatare ulipelekwa Youtube, badala ya kwenye vyombo vya sheria.

Maneno ya Michuzi kwamba ni TISS imeibua hiyo video yanathibitisha ushiriki wa TISS kwenye mchezo huo mchafu, na kwamba Chadema kinajua kuwa Michuzi alishirikiana na watu wa usalama wa taifa katika kazi hiyo chafu. Software za video (editing) walizotumia zilitoka kwake. Fedha ya kuandaa hiyo video zilitoka usalama na Ikulu. Tunajua kuwa wale vijana wa Ada Estate na yule jamaa anayempelekea kigogo wa Jamii Forum, walilalamika sana kwa mmoja wa wamiliki wa JF.

Ndugu waandishi wa habari;
Chadema kinajua kuwa mmoja wa watuhumiwa hawa, Mwigulu Nchemba anafanya mipango na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom ili kumsaidia kufuta taarifa zake. Nachukua nafasi hii, kuionya kampuni hiyo kuacha kucheza mchezo huo kwa kuwa ni kinyume cha sheria za mamlaka ya mawasiliano (TCRA).

Tunahitaji mawasiliano haya kwa kuwa Mwigulu – zinaonyesha mtuhumiwa huyo akifanya mawasiliano mfululizo na Ludovick, yakiwamo yale ya tarehe 4 Machi 2013. Hii ilikuwa siku moja kabla ya Kibanda kutekwa.

Ndugu waandishi wa habari;
Hawa niliowataja ni watu muhimu sana katika upangaji wa mkakati wa utengenezaji wa video ya Lwakatare na vitendo vya kihalifu vya utekwaji wa Kibanda na tukio la kutekwa na kisha kutupwa msutuni kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari nchini, Dr. Steven Ulimboka.

Kwa mfano, simu ya Mwigullu Nchemba, namba 0714 xxxxx, 0756 xxxxx na 0757 xxxxx, zimefanya mawasiliano mara kadhaa na Ludovick Joseph, Saumu K. Malungu, Jack Zoka, Ali Shaali na Ramadhani Ighondo. Mawasiliano hayo yalifanyika katika kipindi ambacho mgomo wa madaktari ulishamiri; baadaye yakarudi tena kati ya 26 Desemba mwaka jana na 15 Machi mwaka huu.

Miongoni mwa mawasiliano ambayo tunaona yanahusika na ujambazi huu, ni yale ya 28 Desemba, siku ambayo mkanda wa Lwakatare umerekodiwa; tarehe 4 hadi 6 Machi 2013, siku moja kabla ya Kibanda kutekwa na yale ya usiku wa manane (saa 8:17) wa 13 Machi 2013, ambako mchana uliofuata Lwakatare alikamatwa.

Huyu Mwagha ndiye aliyekuwa anatumika kuwasiliana na Saumu Malungu, ambaye tulimtaja kuwa ndiye aliyekuwa amepewa kazi na Mwigulu na usalama wa taifa, kurubuni vijana wetu kwa fedha ili kutoa ushahidi wa uongo juu ya video ya Lwakatare.

Vilevile, mawasiliano ya Mwiguluna Mwagha, katika kipindi hicho nayo tunayahitaji. Kwa sababu, huyu Mwagha anayetumia simu 0754xxxxx, mbali na kuwasiliana na Mwigulu, ndiye aliyekuwa anawasiliana na mmoja wa waliomteka Ulimboka; na ndiye aliyewasiliana na Saumu kati ya 20Januari na Machi 6 mwaka huu.

Ndugu waandishi wa habari;
Ludovick alifanya mawasiliano ya mwisho na Joyece Agustine, ambaye anatumia simu Na. 0717 xxxxx, mawasiliano ambayo yalifanyika saa 5:13 usiku. Hiyo ndiyo ilikuwa simu yake ya mwisho usiku huo; katika siku hiyo Ludovick aliwasilisna na Joyce mara tisa kuanzia saa 12: 54 asubuhi.

Kwa mujibu wa taarifa za kwenye mtandao wa Jamii Forum, ambako video ya Lwakatare ilitumwa, Ludovick alikamatwa Machi 15 mwaka huu. Hata hivyo, rekodi katika simu yake Na. 0715 xxxxx inaoyesha 17 Machi Ludovick alifanya mawasiliano na Joyce Augustino. Mawasiliano hayo yalifanyika saa 8: 9 usiku, wakati inadaiwa na polisi alishakamatwa.

Naye mhariri wa Mwananchi, Bw. Msaky ambaye anatajwa kutaka kutekwa na Ludovick na Lwakatare, amekuwa na mawasiliano kadhaa na Ludovick – mtu anayepanga kumteka. Ludovick na Msaky walifanya mawasiliano mfululizo kati 27 Desema 2012, siku moja kabla ya video ya Lwakatare haijarekodiwa na 7 Machi siku moja baada ya Kibanda kutekwa.

Msacky alitumia simu zake hizo mbili (0764 xxxxx na 0655 xxxxx) kuwasiliana na Ludovick, huku Ludovick akitumia 0753xxxxx. Mawasiliano ya 31 Desemba yalifanyika Ludovick akiwa Tegeta, jijini Dar es Salaam. Mawakala hawa wawili wa usalama wa taifa (Ludovick na Msaky), walikutana 31 Desemba 2012, katika hoteli ya Tamal, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ndugu waandishi wa habari;
Baada ya kupitia taarifa hizi za mawasiliano ya simu za Mwigulu Nchemba, Ludovick Joseph, Ramadhani Ighondo na Saumu Malungu tumegundua yafuatayo: Kwamba, Ramadhani Ighondo, amefanya mawasiliano mara nyingi na Mwigulu, Mwagha na Zoka; naye Mwagha amefanya mawasiliano na Mwigulu na Saumu; naye Saumu amefanya mawasiliano na Mwagha, Mwiguluna Shaali Ali, ambaye ni afisa usalama wa taifa.

Tumegundua vilevile, kuwapo mawasiliano kadhaa kati ya Ludovick na Msaky; Ludovick na Mwigulu; Msaky na Nchimbi; Msaki na Mwagha, Samu na Mwagha na Ramadhani Ighondo Abeid, anayetuhumiwa kumteka Dk. Ulimboka na Mwanga na Mwigullu.

Tumegundua pia kuwapo mawasiliano kati ya Ulimboka na Ramadhani; Zoka na Ighondo na Ridhiwani na Ighondo. Mawasiliano haya yalifanywa mfululizo usiku wa Juni 2012 siku ambayo Dk. Ulimboka alitekwa.

Tumepata kufahamu pia kwamba baadhi ya watu waliotajwa na gazeti la MwanaHALISI kuwa waliwasiliana na Ighondo usiku wa Juni 26, mwaka 2012, wamefanya mawasiliano pia na Mwigulu, Mwagha na Shaali Ali.

Ndugu waandishi wa habari;
Mwagha ni afisa usalama wa taifa anayefanyakazi makao makuu ya idara hiyo. Ndiye yule anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga wanasiasa wa CCM na upinzani. Ni Mwagha anayepanga wabunge na kuwapanga waongee nini kwa maslahi ya CCM. Ushenzi wote anaoongea Mwighulu bungeni, hupewa na Mwagha kwa maelekezo ya Jack Zoka.

Naye Shaali ndiye aliyekutana na afisa wetu wa usalama, Ahmed Sabula na mwenzake, Machi 29 mwaka huu katika hoteli ya See Cliff jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo kati ya Sabula, kijana wetu wa usalama na afisa usalama wa serikali Bw. Shaali alitaka Sabula akubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya chama, kuwasilisha kwake nyaraka za kamati kuu na kueleza mipango ya chama katika kesi ya Lwakatare.

Kwenye mpango huu, afisa huyo wa usalama wa taifa ambaye ninamfahamu vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha Sh. milioni 30 na kwamba fedha hizo angelipwa wiki iliyopita. Aliahidiwa pia kwamba kila nyaraka atakayopeleka atalipwa ujira.

Aidha, Sabula aliahidiwa kulipwa shilingi 500,000 (laki tano) kila mwezi; afisa wetu huyu ameripoti tukio hilo kwa viongozi wake wa chama. Yule mwenzake aliandaliwa kuwa shahidi wa kesi ya Lwakatare; aliambiwa akikubali dili hiyo atalipwa kila mwezi Sh. 500, lakini akaombwa kuwa mvumilivu kwa kuwa atalazimika kupotea kwa miezi kama mitano hadi sita.

Ndugu waandishi wa habari;
Kitendo cha Mwigulu kuwasiliana Ramadhani Ighondo, Mwigulu kuwasiliana na Ludovick, Saumu kuwasiliana na Mwigulu, Ighondo kuwasiliana na Ulimboka, Zoka kuwasiliana na Ighondo, tena katika muda uleule ambao Ighondo amewasiliana na Ulimboka na Saumu kuwasiliana na Mwagha, ni uthibitisho tosha kwamba usalama wa taifa wako nyuma ya mipango hii ya michafu ya kupanga utekaji na kisha kutaka kukichafua Chadema.

Aidha, kitendo cha Ludovick kuwasiliana Msaky; Ighondo kuwasiliana na Mwagha, Ridhiwani Kikwete kuwasiliana na Ighondo, tena kila baada ya Ighondo kuwasiliana na Ulimboka na Jack Zoka, ni uthibitisho mwingine kuwa genge hili la wahalifu linashirkiana na baadhi ya watu kutaka kuangamiza taifa.

Ni uthibitisho tosha kwamba hawa ndiyo wanaowahonga wanachama wa Chadema na watu wengine ili watoe ushahidi feki dhidi ya Lwakatare, na kwamba ni usalama wa taifa walioandaa ile video uchwara inayopigiwa chapuo na Mwigulu.

Ndugu waandishi wa habari;
Chama Cha Mapinduzi kinajua kwa hali ya sasa hakiwezi kushinda uchaguzi wa mwaka 2015 huku Chadema ikiwa katika hali nzuri ya kisiasa tunayoiona sasa. Wanajua kabisa CCM imegawanyika, kundi lolote litakalopita ndani ya CCM, litahujumu kundi jingine. Ni kama ilivyotokea uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki.

Ndiyo maana wanapanga kila mbinu kutaka kuiangamiza Chadema. Nasi tunasema katu hatutakubali kuona Chadema kinakufa. Tutapambana usiku na mchana. Juna na mvua. Hadi tushinde hila hizi.Tunawaambia wanachama wetu na wale wanaotuunga mkono, Chadema ni chama kikubwa. Kina mtandao kila mahali, kuanzia Ikulu hadi polisi; na hivyo hakitakufa au kuzorota kwa mambo ya kupikwa.

Ni imani yangu kwamba amri ya mahakama itawafichua wote hawa ni kuirudisha Tanzania katika amani yake. Ni lazima tufikike mahala watu hawa wafahamike mbele ya umma, tunataka wafahamu kuwa maisha ya mwanadamu yana thamani kuliko siasa chafu na ufisadi wanaouendeleza.

Nawashukuru kwa kunisikiliza.

Mabere Marando,
Dar es Salaam

Monday, April 1, 2013

HOTUBA YA RAIS MWEZI MACHI 2013

-
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. Leo ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa China Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Jambo la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe wake. Wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu wake.

Kwa niaba yenu, nimepokea salamu za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa na mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku za usoni.
Ndugu wananchi;
Nami pia, nimemshukuru sana Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa na kumbukumbu isiyosahaulika. Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake. Na, kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi wake.
Tumefarijika sana kusikia kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi wapya wa China. Pia, kuwa China itaendelea kukuza biashara na uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000 za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi zetu mbili zilitiliana saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya kipaumbele nayo imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais Xi Jinping alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti cha China ya kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China. Kama mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na Waziri Mkuu wake Chou En Lai.
Rais wa China aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa na kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada ya maendeleo. Katika miaka 49 ya uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo ikiwemo Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na Rais Xi Jinping wakati wa ziara yake.
Ndugu wananchi;
Kuna miradi kadhaa mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa Serikali ya China. Wakati wa ziara yake, Rais Xi Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo kama tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku ile.
Ajali ya Kuporomoka Jengo la Ghorofa
Jijini Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la Dar es Salaam. Ajali hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana. Watu 17 waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na sasa inakaribia kufikia ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Mimi na viongozi wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona pale imenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti. Pia nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hii. Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi. Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile. Alimradi kila mtu ana dhana yake. Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua zipasazo. Wa kushtakiwa Mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe bila ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu wake. Naamini kama mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika. Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao. Watimize wajibu wao. Yaliyotokea Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote.

Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli ujulikane. Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe. Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha ajali za aina hiyo siku za usoni.
Uhusiano wa Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini. Jambo hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa. Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya. Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga Makanisa na shule za Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo wote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati mbalimbali. Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali. Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.

Ndugu Wananchi;
Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale ambapo sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi wa dini na nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini hivyo sivyo. Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.

Kila tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali kuzembea. Hakuna ushahidi wa matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa hatujapata ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si tukio unaloweza kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale pale Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu zao.

Hivi kama kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao. Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili. Busara ituongoze kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze, waelewane na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali. Hata mzozo wa kuchinja wanaweza kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo na watu hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na Waislamu nchi nzima si sawa. Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la Buseresere, Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje. Bado uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi. Tumefanya hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla yake. Yaani ile la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga. Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo. Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu? Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua fumbo hilo.
Kuna watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika. Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje. Katika mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu ya kufanya hivyo. Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina mazingira yake maalum. Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran Tukufu. Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu. Kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa. Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale, wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
Baada ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli. Hata dalili hazijakuwepo.
Tulichojifunza ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu. Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa faida yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na Waislamu wagombane. Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake. Ni mchezo mbaya, tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati ya Wakristo na Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani. Kwa upande wa tukio la Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar, watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma Kanisa baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika pamoja na kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua hatua. Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za kidini. Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama wa raia wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi zote na mahali po pote walipo wako salama. Tunataka kuona watu wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku zote. Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha. Tujiepushe kuyapa kipaumbele yale yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na maeneo mengine yenye huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena. Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na wakati ni huu. Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na janga hili.
Ndugu Wananchi;
Bado narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye majawabu ya matatizo haya. Ni masuala yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao. Serikali ina wajibu wa kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi baya ni viongozi wa dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo hilo. Nimepata faraja kuona kuwa wote wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza. Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa Tanzania na Watanzania. Kuna upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake katika maisha tuliyoyazoea. Maisha ambayo waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao. Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya kutuma wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika au kuzitangaza. Wawe makini na maneno wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote. Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha umoja na mshikamano wetu. Tuishi kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu, kabila, rangi au mahali atokako mtu. Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini yo yote na wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini wao. Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi. Hatua zipasazo zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na utulivu. Tusherehekee pamoja.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

Tuesday, February 5, 2013

Hoja binafsi ya John Mnyika iliyokataliwa jana Bungeni






Mheshimiwa Spika;
Awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wa kuwawakilisha wananchi, kuisimamia serikali, kuidhinisha mipango na kutunga sheria.

Mheshimiwa Spika;
Aidha, kwa namna ya pekee ni kushukuru wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge kwa kunipa fursa hii adimu na adhimu ya kuwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni ya 54 fasili ya (1) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika;
Maji ni uhai, hivyo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na nchini kwa ujumla kama hatua za haraka zisipochukuliwa yatageuka kuwa janga la taifa. Katika kila watanzania katika Jiji la Dar es Salaam na nchini; kwa wastani mmoja hapati huduma ya maji safi na salama na hali ni mbaya zaidi kuhusu ushughulikiaji wa maji taka.

Wakati baadhi ya nchi duniani zikielezwa kwenye kitabu cha hivi karibuni cha Mnukuzi Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN Special Rapporteur) kuwa katika mwelekeo unaostahili kuhusu kuhakikisha haki ya maji na usafi wa mazingira (On the right track; Good practices in realizing the rights to water and sanitation: 2012), hali ni kinyume kwa taifa letu.

Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya maji (WaterAid: 2011) imeiweka Tanzania katika kundi la nchi ambazo haziko katika mwelekeo unaostahili wa kuboresha upatikanaji wa maji safi, ushughulikiaji wa maji taka na usafi wa mazingira (Policy Report: Off Track, Off Target; why investments in water, sanitation and hygiene is not reaching those who need the most).

Mheshimiwa Spika;
Hoja hii inalengo la kuibua mjadala wa hatua za haraka. Kimsingi hatua hizi za haraka hazitanufaisha Mkoa mmoja pekee kwa kuzingatia kuwa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam ni kwa ajili pia ya maeneo mengine ya miradi iliyo sehemu ya mpango huo ya Morogoro mpaka Pwani. Aidha, kujadiliwa na kupitishwa kwa mapendekezo ya hoja hii kutaongeza pia msukumo wa miradi katika maeneo mengine ya mijini na vijijini katika mikoa mbalimbali nchini.

Shukrani zangu za dhati ziwafikie wabunge wenzangu wa vyama vya upinzani na wa chama tawala kwa maoni na mapendekezo yenu yaliyoniwezesha kuirekebisha hoja hii pamoja na ushauri wa Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashillilah na maafisa na watendaji katika ofisi ya bunge, kambi rasmi ya upinzani na ofisi ya mbunge wa Jimbo la Ubungo mlioboresha hoja hii kwa manufaa ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika;
Nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi mnaoendelea kuniunga mkono kwa hali na mali katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge na nafasi nyingine ninazozitumikia.

Nawashukuru sala zenu wakati wa kesi ya msingi na rufaa ya kupingwa kwa matokeo ya ushindi wetu Jimbo la Uchaguzi la Ubungo; kwa pamoja tumeshinda, tuendelee na kazi.

Aidha, pamoja na mjadala huu wa bungeni natarajia kupokea maoni na mapendekezo yenu kuhusu hoja hii kwa njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo kupitia mtandao wa http://mnyika.blogspot.com kwa hatua zaidi. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.

MAELEZO YA HOJA:

Mheshimiwa Spika;
Maji ni mojawapo ya mahitaji ya msingi ya binadamu, maji ni uhai. Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni sehemu ya muhimu ya maendeleo ya nchi na maisha ya wananchi. Maji ni lazima kwa matumizi ya majumbani, maji ni muhimu ni moja ya malighafi muhimu katika kazi za uzalishaji iwe ni za viwanda, kilimo, mifugo na shughuli zingine za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa vyanzo vingi vya maji, vinavyohusisha mito, mvua, maziwa na bahari; kuwepo kwa vyanzo hivi vya maji ni wazi kuwa nchi yetu inaweza kuepukana na shida ya maji inayoikumba jamii ya Tanzania iwapo tutaondoa udhaifu uliopo. Aidha, udhaifu huo unahusisha pia kuziweka vyanzo vyenyewe pia mashakani kwa matendo ya binadamu yenye kuathiri endelevu wa matumizi hali itayozua migogoro katika siku za usoni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika;
Upatikanaji wa maji safi na salama kwa urahisi wa bei unachangia katika kupunguza gharama za maisha; upatikanaji wa maji safi na salama karibu na makazi husaidia jamii, hususan wanawake, kutumia nguvu na muda katika uzalishaji na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini. Upatikanaji wa maji safi na salama ni nyenzo ya kulinda utu na afya; kinyume chake kuenea kwa magonjwa na maisha duni.

Ifahamike kuwa kadiri ya Tathmini ya Hali ya watu na Afya ya mwaka 2010 (Demographic and Health Survey 2010); ni asilimia 4.8 tu ya kaya zilizopo vijijini ndiyo zinazopata maji katika eneo lao la kaya (water on premises) wakati ni asilimia 19.4 tu ya kaya kwa mijini ndizo zenye maji katika kaya zao. Hivyo kaya nyingi za Tanzania zinawekwa katika mazingira hatarishi kwa magonjwa ya mlipuko na mengine ambayo si ya mlipuko kutokana na uhaba wa maji, hali ikiwa tete zaidi katika maeneo yasiyopimwa yenye msongamano mkubwa wa watu katika Jiji la Dar es Salaam (slums).

Mheshimiwa Spika;
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, toleo la mwaka 2005 haijataja haki ya kupata maji safi na salama; huu ni kati ya upungufu ambao wananchi wa mijini na vijijini wanapaswa kuutolea maoni katika mchakato wa katiba mpya kwa kurejea mfano wa Katiba ya Afrika Kusini, Ghana na katiba mpya ya Kenya.

Katika hatua ya sasa haki hii inapaswa kulindwa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (“The International Covenant on Economic, Social and Cultural Rights”, ICESCR) wa 1966. Mkataba huu unataja haki za kijamii na hivi karibuni Umoja wa Mataifa (UN) umeutafsiri kuwa ni pamoja na haki ya kupata maji safi na salama ambayo inapaswa kutiliwa mkazo katika nchi yetu.

Suala la upatikanaji wa maji safi na kuweza kushughulia maji taka ni sehemu ya makubaliano ya kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia kuingia mathalani Malengo ya Milenia (MDGs); lengo namba saba (7) shabaha 10; la kupunguza nusu ya watu waoishi bila maji na safi ya kunywa na usafi wa msingi. Hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka ni muhimu kama sehemu ya haki za binadamu lakini lina tija pia katika uzalishaji na uchumi wa nchi kwa kuwa tafiti zinaonyesha kwamba kudumu kwa matatizo hayo kunazigharimu nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo wastani wa asilimia sita (6) ya pato la taifa (Gross Domestic Product).

Utafiti uliofanywa kwa Stockholm Environment Institute kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika mwaka 2006 kuhusu uhusiano kati ya maji na umaskini Afrika kwa kutumia mfano wa nchi yetu (Water and Poverty Linkages in Africa: Tanzania Case Study) umebainisha namna ilivyo vigumu kupima Tanzania inavyosonga mbele katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia yanayohusu maji. Aidha, utafiti huo umeeleza namna ambavyo bila kushughulikia kwa haraka matatizo ya maji jitihada za kupambana na umaskini zitakwama.

Mheshimiwa Spika;
Jiji la Dar es Salaam ni letu sote, ni mahali ambapo wabunge wote tunaishi kwa nyakati mbalimbali hususan wakati wa vikao vya kamati za kudumu za Bunge hivyo adha ya maji katika Jiji hili kila mmoja anaifahamu na anawajibu wa kushiriki katika kuipatia ufumbuzi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2002 Mkoa wa Dar es salaam ulikuwa na jumla ya wakazi 2,497,940 huku ukikadiriwa kuwa na kasi ya ongezeko la watu ya asilimia 6 kwa mwaka; ikiwa ni juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.5, lakini kasi ya upatikanaji wa maji na ushughulikiaji wa maji taka ikiwa ndogo. Bunge ikiwa ni chombo cha juu cha kuisimamia Serikali linapaswa kuitafakari hali hii kwa upekee wake kwa kuwa itakuwa na athari kwa taifa kwa sasa na baadaye ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

Hadi kufikia mwaka 2011 Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na watu zaidi milioni nne na laki tano likiwa na takribani nusu ya waajiriwa wote wa viwandani nchini. Hivyo kwa kurejea takwimu za ujumla za sensa zilizotolewa mwezi Desemba 2012 kwamba Tanzania kwa sasa ina watu zaidi ya milioni 44.9; hoja hii inalenga kupendekeza kwa bunge kujadili kuhusu mustakabali wa zaidi ya asilimia 10 ya Watanzania, lakini kwa kurejea utangulizi wangu maazimio ninayopendekeza yapitishwe yatakuwa na maslahi sio kwa wakazi wa Dar es salaam bali kwa taifa kwa ujumla mijini na vijijini.

Mheshimiwa Spika;
Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.

Zipo hisia kwamba Dar es salaam inapata huduma maji safi na maji taka kuliko miji na mijiji mengine nchini, lakini uhalisia unaonyesha kwamba hali ni bora kwa wachache wakati walio wengi hususan waoishi kwenye maeneo ya wananchi wa kipato chini hali ya upatikanaji wa maji ni duni kuliko miji na majiji mengine nchini.

Jiji la Dar es Salaam ni la mwisho kwa kigezo cha wastani wa kitaifa wa upatikanaji wa maji ukilinganisha na majiji mengine ambayo yanafikia asilimia 75; hivyo hatua za haraka zinahitajika kurekebisha hali hiyo.

Hatua hizo zitawezesha kupunguza kwa haraka tatizo hilo na kuelekeza nguvu zote katika maeneo ya vijijini palipo na shida kubwa badala ya mfumo wa sasa ambapo kwa miaka zaidi ya kumi, rasilimali zinatumika lakini kunakosekana ufumbuzi endelevu maeneo yote.

Hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kuhusu hali hii kwa kuzingatia kuwa idadi ya watu katika Jiji la Dar es salaam inaendelea kukua kwa kasi likiwa ni jiji la tatu kwa ongezeko kubwa la watu barani Afrika na la tisa duniani; matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika jiji kutokana na msongamano wake wa watu ni bomu la wakati.

Mheshimiwa Spika;
Mkoa wa Dar es Salam unapata maji kutoka mito na visima kwa matumizi ya nyumbani, viwanda, bustani, mifugo, usafi na Mazingira. Sehemu ya Jiji inayopata maji inahudumiwa na Kampuni ya DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage Company) ambayo imepewa mkataba na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam, DAWASA (Dar es Salaam Water Supply and Sewerage Authority) na maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, Taasisi na watu binafsi.

Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Jimbo la Ubungo kama sehemu ya Jiji la Dar es salaam katika kufuatilia masuala ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi. Nikiri kwamba katika hatua za awali ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’ kwenda DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa DAWASCO ambapo nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji. Wakati wa hatua hizo tumewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya maji iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji wao; hatua zaidi zinahitajika.

Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwito wa mara kadhaa hapa bungeni; nashukuru pia Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe alifika Jimboni Oktoba 2012 kwa ajili ya uzinduzi wa visima katika maeneo ya King’ongo, Kilungule na Mavurunza na kuona hali halisi ya ugumu wa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es salaam.

Natambua pia jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji (BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba. Hata hivyo, yapo bado maeneo mengi yenye matatizo makubwa ya maji ikiwemo ya Msumi, Makabe, Msakuzi, Malambamawili, Msingwa, Goba na mengineyo mengi katika Jiji la Dar es salaam. Na hata yale yenye miundombinu ya maji kama Sinza, Manzese, Makurumla na mengine nayo hali ni tete. Hali iko hivyo katika Manispaa zote tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke.

Mheshimiwa Spika;
Hata katika maeneo ya umma ya kuuzia maji, bei ipo juu kwa kuwa mamlaka zetu za kuratibu na kusimamia masuala ya bei kama EWURA imekuwa na udhaifu katika kusimamia na kuratibu bei elekezi wanazozitoa. Kwa mfano jiji la Dar es Salaam: vituo vingi vya kutoa huduma za maji chini ya DAWASCO/DAWASA maarufu kama “vioski vya maji” vimekuwa vikiongeza bei tofauti na bei elekezi toka EWURA ya Tsh 1 kwa lita moja yaani ndoo ya lita 20 kwa Sh 20 kinyume na waraka nambari 10-017 (Order No.10.017) wa Juni 8, 2010, agizo lililopaswa kuanza kutekelezwa Juni 15, 2010.

Utafiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Twaweza uliofanywa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam uliopewa jina; “Bei ya maji Dar es Salaam Je, wanaoendesha maghati ya maji wanazingatia bei walizopangiwa?” uliweza kubainisha kukithiri kwa bei zilizoongezwa kinyume na taratibu na agizo hilo la EWURA katika maghati ya maji. Hata baada ya kurekebishwa kwa agizo hilo na bei kuongezwa kiasi bado maeneo hayo ya kuuzia maji kwa umma yamekuwa yakipandisha bei kupindukia.

Mheshimiwa Spika;
Kero kubwa zaidi iko wa wauzaji binafsi ambapo mazingira ya upungufu na ukubwa wa mahitaji umefanya maji yauzwe kama bidhaa ya anasa bila mamlaka EWURA kutunga kanuni wala kudhibiti bei, na kuachia soko holela yenye kuambana na hujuma za miundombinu katika baadhi ya maeneo ili kuongeza uhaba.

Wananchi ambao wengi wao ni wa kipato cha chini hupata huduma ya maji kwa gharama kubwa ambayo huuzwa kwa kati ya Tsh 300 hadi Tsh 500 kwa ndoo ya lita 20 kwa maeneo ya Dar es salaam.

Kuwapo pia kwa watoa huduma wasio rasmi husababisha bei ya maji kuwa kubwa ambapo inakadiriwa kuwa 68% ya wakazi wanaoishi maeneo ya mjini yenye msongamano mkubwa hupata maji kutoka kwa wauzaji wasio rasmi.

Hatua za haraka zinahitajika kudhibiti ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo wanaonunua maji kwa madumu hununua bei ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata huduma ya maji ya bomba.

Mheshimiwa Spika;
Kwa nyakati mbalimbali katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 mpaka 2012 Serikali imekuwa ikitoa ahadi bungeni ya kumaliza tatizo la majisafi na majitaka katika Jiji la Dar es Salaam bila utekelezaji sahihi, kamili na wa haraka.

Malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini wa kwanza (MKUKUTA I) yaliyoingizwa pia katika ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2005-2010 hayakuweza kutekelezwa.

Malengo mengine yameingizwa katika ilani ya CCM na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini awamu ya pili (MKUKUTA II) ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira ifikapo mwaka 2015; nayo tukiwa mwaka 2013 mwelekeo unaonyesha kwamba hayatafikiwa iwapo hatua za haraka zisipochukuliwa.

Mara baada ya kupitishwa kwa Mpango Maalum wa Maji katika Jiji la Dar es salaam mwaka 2011, Rais alitangaza kwamba tatizo la maji kuwa historia mwaka 2013; ambapo ni mwaka huu. Hata hivyo, utekelezaji wa mipango hauashirii ahadi hiyo kutekelezeka na kwa mwelekeo wa sasa tatizo litaendelea mpaka baada ya mwaka 2016 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika;
Mabomba ya ‘mchina’ bila maji na miradi hewa katika maeneo ya wananchi wa kipato cha chini Jijini Dar es Salaam:

Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP).

Mradi huo uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

Hali hii ni kati ya matatizo yanayokera wananchi wa Jiji la Dar es salaam kwa kuwa na mabomba yasiyotoa maji kwa muda mrefu hata kwa mgawo maarufu mitaani kama mabomba ya ‘mchina’.

Serikali ilieleze bunge lako sababu ya mabomba hayo kutokutoa maji mpaka hivi sasa, lini mabomba hayo yataanza kutoa maji katika maeneo ambayo maji hayatoki mpaka sasa na hatua gani zimechukuliwa wa waliotekeleza mradi huo bila kuzingatia maandalizi ya msingi.

Ni muhimu hatua zikachukuliwa kwa wahusika kwa kuwa kitendo cha mabomba hayo kukaa muda mrefu bila kutoa maji inafanya miundombinu hiyo kuanza kuharibika au kuharibiwa ambayo ni hasara kwa taifa kwa kuwa pamoja na fedha zilizotumika kuweka mabomba hayo kupotea, fedha nyingine zitatumika katika hatua ya baadaye kufanya matengenezo kwenye maeneo yaliyoharibika.

Aidha, yapo pia malalamiko ya kwamba yapo maeneo ambayo yalitoa maji mara chache kati ya mwaka 2009 na 2010 lakini baada ya hapo maeneo hayo hayajatoa maji tena mpaka sasa, Serikali itoe maelezo ya kitaalamu kwa bunge na kwa wananchi kuhusu sababu za maji hayo kutoka wakati huo na kutokutoka tena na hatua zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo.

Mheshimiwa Spika;
Kasoro katika mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP); hazielezwi na wananchi pekee bali pia hata watafiti mbalimbali.

Ripoti ya karibuni kabisa mwaka 2012 ya Shirika la Kimataifa la Water Aid ya utafiti uliofanywa ukihusisha wataalamu kutoka Overseas Development Institute na Chuo kimoja cha nchini Uingereza (SOAS) iliyofuatilia uwekezaji wa miradi ya maji mijini katika nchi za Ghana, Burkinafasso na Tanzania ( Stregthening pro poor targeting of investments by African utilities in urban water and Sanitation) ikiwemo namna miradi ilivyoshindwa kuwajali maskini na maeneo na kiwango cha hali ya maji kutokupatikana kinyume na malengo yaliyowekwa wakati wa kuanza kwa mradi.

Mheshimiwa Spika;
Matatizo ya kuwa na mabomba yasiyotoa maji hayapo tu katika mabomba waliyofungiwa wananchi majumbani bali pia kwenye visima na ‘vioski’/maghati ya jumuiya. Kuna udhaifu wa kuanzisha miradi ya jamii na kuacha kusimamia uendelevu (sustainability) wake na hatimaye baada ya muda mfupi miradi hiyo iliyotumia fedha za umma inabaki kuwa ‘miradi hewa’.

Utafiti wa vituo vya maji uliofanywa June 2009 na Overseas Development Institute (ODI) chini ya udhamini wa shirika la Water Aid hapa nchini ulibainisha ni asilimia 54 tu ya vituo vya maji vilivyopo ndivyo vinatumika kwa kutoa huduma ya maji.

Hivyo kwa wastani baada ya miaka miwili tu ya kujengwa karibu nusu ya visima na vioski huwa haviendelei tena kufanya kazi. Utaratibu wa kukimbilia kutumia fedha za miradi ya maji kwa mwaka wa kibajeti mpya bila kuzingatia taarifa za utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi ya nyuma ni hatari kwa uendelevu wa kuwepo kwa huduma ya maji kwa siku zijazo kama hatua za haraka hazitachukuliwa kuzingatia matatizo yaliyojitokeza katika miradi iliyopita na kuzingatia ubora na ufanisi katika miradi ya maji nchini.

Mheshimiwa Spika;
Utafiti uliofanywa na Economic and Social Research Foundation, umebaini utofauti wa utekelezaji wa miradi ya serikali na mashirika binafsi katika kauhakiki ubora wa matumizi ya fedha na huduma kwa jamii. Utafiti ulibaini kuwa katika miradi iliyofadhiliwa na mashirika ya maendeleo, wastani wa asilimia 67 ya vioski vilionekana kufanya kazi; wakati miradi ambayo imefadhiliwa na Serikali ni wastani wa asilimia 45 ya vioski vya maji vilikuwa vikifanya kazi katika maeneo hayo hayo. Utafiti huo ulihusu Mikoa ya Singida na Dodoma.

Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa utafiti mwingine wa Shirika la Water Aid uliobainisha kuwa asilimia 85 ya vioski vilivyounganishwa Jijini Dar es Salaam havitoi maji, Asilimia 10 vinatoa maji kwa kusuasua na asilimia 5 tu ndivyo ambavyo vinatoa maji kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika;
Kasoro katika utendaji na uwajibikaji wa mamlaka na vyombo vinavyohusika na utoaji na udhibiti wa huduma ya maji:

Majukumu ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam na baadhi ya maeneo ya Kibaha na Bagamoyo yanafanywa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) ambayo ni mmiliki, mkodishaji na msimamizi wa utoaji wa huduma ya majisafi na maji taka na ina wajibu wa kupanga na kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuiendeleza na kugharamia matengenezo ya dharura na makubwa.

Mwaka 2005 DAWASA iliingia mkataba wa miaka kumi (10) wa uendeshaji na Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO). Chini ya mkataba huo majumu ya DAWASCO ni kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na uondoshaji wa maji taka, kuuza maji kwa wateja , kutoa ankara kwa wateja, kukusanya maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji, kutekeleza matengenezo makubwa yanayogharamiwa na DAWASA na kutekeleza uunganishaji wa maji kwa wateja wapya kwa kutumia mfuko wa maji.

Kisheria na kimkataba DAWASA ina wajibu wa kuisimamia DAWASCO iliyoingia nayo mkataba; hata hivyo kwa kuwa yote ni taasisi na mashirika ya umma ambayo bodi zake na watendaji wake wakuu huteuliwa na mamlaka zile zile na kuripoti kwa watu wale wale, hali ambayo ina athari kwenye utendaji na uwajibikaji.

Wakati umefika sasa wa mkataba huo kati ya DAWASA na DAWASCO kuwekwa wazi kwa umma; kufanyiwa tathmini ya miaka zaidi ya mitano iliyopita ya utekelezaji; kufanyiwa marekebisho kwa ajili ya kipindi kilichobaki na maandalizi kuanza ya mfumo bora unaopaswa kuanza kuandaliwa baada ya kuisha kwa mkataba huo mwaka 2015.

Utoaji wa huduma ya maji unamhusu pia mdhibiti ambaye ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) yenye mamlaka ya kudhibiti utoaji wa huduma, kuidhinisha bei ya huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka pamoja na kutoa leseni za uendeshaji. Hata hivyo, EWURA imekuwa ikitoa kipaumbele zaidi kwenye kutumia mamlaka yake kudhibiti kwa karibu sekta ya nishati, huku udhibiti kwenye sekta muhimu ya maji hususan kwa upande wa watoa huduma binafsi ukiachwa uwe katika mfumo wa soko holela na kuchangia katika ongezeko la bei ya maji pamoja na ubovu wa huduma.

Wakati umefika sasa wa Bunge kusimamia kwa karibu utekelezwaji wa The Energy and Water Utilities Regulatory Authority Act (Sura ya 414) kifungu cha 6 ambayo inaelekeza bayana kwamba wajibu wa EWURA ni pamoja na kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma inazozidhibiti ikiwemo maji wa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio pembezoni au katika mazingira magumu (low income and disadvantaged consumers).

Aidha kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha sheria hiyo majukumu ya EWURA ni pamoja na kupanga viwango cha ubora, viwango vya ugavi, kufuatilia utendaji ikiwemo uwekezaji na upatikanaji, kudhibiti bei na tozo na kushughulikia malalamiko na migogoro.

EWURA itumie mamlaka yake pia kwa kutumia vifungu vya 16, 17, 18 na 19 kuhakikisha kwamba masuala ya udhibiti wa bei hashaishii tu katika mamlaka za umma na pia ianze yenye uchunguzi juu ya kuporomoka kwa kiasi na kiwango cha huduma za maji katika Jiji la Dar es salaam na nchi kwa ujumla na kupendekeza hatua za ziada za haraka zaidi kuweza kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika;
Mwaka 2011 Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi wa ufanisi (performance audit) kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini ikiwemo Dar es salaam, hata hivyo taarifa yake ya Januari 2012 baada ya kutajwa bungeni miongoni mwa hati zilizowasilishwa; hatua za kutekeleza mapendekezo yake hazikupata usimamizi wa kutosha wa kibunge.

Hivyo, ipo haja kwa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa niaba ya Bunge ipokee maelezo ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo ambayo yalilenga kuboresha utendaji wa DAWASA, DAWASCO na Mamlaka zingine za maji katika mikoa yote nchini na hatimaye kamati hiyo iwasilishe maoni na mapendekezo yake bungeni kwa ajili ya hatua zaidi.

Mfumo duni wa ushughulikiaji wa maji taka ni bomu la wakati katika Jiji la Dar es salaam:

Mheshimiwa Spika;
Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia 10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam, mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Kwa mujibu wa ripoti ya EWURA ya mwaka 2009, viwango vya huduma za uondoaji maji taka katika asilimia vimewekwa katika mabano Mwanza (3.1%), Moshi (5.8%) Arusha (7.0%), Dodoma (11.6%), Tabora (1.3%) na Tanga (9.3%).

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kwa upande wa Dar es salaam huduma za mtandao wa maji taka ni kwa kiwango cha asilimia 4.8 katika Jiji lenye msongamano mkubwa wa watu ambapo hata katika kata zilizopimwa kama ya Sinza na nyinginezo hali ni tete.

Matokeo yake ni kuwawapo wakazi ambao hukiuka sheria na kusubiri mvua zinyeshe na kutiririsha maji taka hali ambayo ni hatari kwa afya za wananchi; kwa upande wa vijijini unafuu unapitakana katika ukubwa wa maeneo ya kuweza kuchimba vyoo, kinyume na mijini ambapo kadiri gharama za kukodi magari ya maji taka kwa sekta binafsi zisizodhibitiwa zinavyozidi kuongezeka ndivyo hatari zinavyozidi katika maeneo wanayoishi wananchi wa kipato cha chini.

Udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri, kamati na jumuiya za watumia maji:

Katika baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo za Jiji la Dar es salaam yamekuwepo matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri kwa kushirikiana na kamati za maji au jumuiya za watumia maji.

Kushindwa kushughulikiwa kwa matatizo ya kimfumo kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji, kutokutekelezwa kwa wakati kwa vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti za Halmashauri iliyopitishwa na madai ya ufisadi katika miradi inayosimamiwa na kamati za maji au jumuiya za watumiaji katika baadhi ya maeneo kumesababisha wananchi kukosa huduma ya maji.

Hata hivyo, pamoja na wananchi kuwasilisha malalamiko yao Wizara ya Maji na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI) ili kutimiza wajibu wa usimamizi na ufuatiliaji hatua za haraka zimekuwa hazichukuliwi hali inayohitaji mjadala na usimamizi wa kibunge.

Katika mjadala utakaotokana na hoja hii, naamini wabunge wenzangu mchangia uzoefu wenu katika maeneo mnayotoka; naomba kwa upande wangu nitoe mfano wa Manispaa ya Kinondoni kuhusu mradi wa maji kata ya Goba.

Tatizo la maji katika kata ya Goba limedumu sasa kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano, pamoja na kwamba serikali inaowajibu kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio pembezoni au katika mazingira magumu mamlaka zinazohusika hazijaweza kutimiza wajibu ipasavyo kuhusu kata ya Goba.

Jitihada nyingi zimefanywa zilizofanywa na wakazi wenyewe kama njia mbadala ya kupata huduma hiyo muhimu kwa maisha ya Binadamu lakini zimekuwa zikikwamishwa na baadhi ya watendaji wa Halmashauri kwa kushindwa kusimamia kwa kurejesha na kupanua huduma hiyo muhimu kwa wananchi hata baada ya kupokea malalamiko katika nyakati mbalimbali .

Mnaweza mkajiuliza sababu za suala hili kuvuka mipaka ya Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni, mpaka Bungeni; ni muhimu ifahamike mapema kwamba jitihada katika ngazi hizo kwa miaka mingi hazijaweza kuleta ufumbuzi hali inayohitaji chombo cha juu zaidi kwa niaba ya wananchi; yaani Bunge kujadili kwa kuwa Wizara ya Maji nayo imeshindwa kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati.

Historia ya tatizo hili inaonesha kuwa wakazi wa Goba wameshawahi kuandika barua kwa Waziri wa Maji barua ya tarehe 15/10/2009 ikieleza kero ya maji kwa wananchi na wakimtaka alipatie ufumbuzi tatizo hilo na nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, na mkuu wa wilaya ya Kinondoni pamoja na hayo bado tatizo linaendelea kutopatiwa ufumbuzi huku wakazi wa Goba wakiendelea kukosa haki yao ya msingi kwa kuwa hakuna maisha bila maji.

Kushindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kulipelekea wananchi pia kuandika barua ya wazi kwa waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda wakilalamikia mradi wa maji wa muda mrefu, pamoja na barua hiyo hakuna jitihada kamili zilizofanyika za makusudi kuondoa tatizo hilo.

Utendaji mbovu na usimamizi mbovu wa miradi ya maji kwa manispaa ya Kinondoni chini ya kamati za maji zilizosababisha maji kukatwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2007 na 2011 ndiyo chanzo cha ukosefu wa maji kwa kipindi chote hicho.

Katika kipindi cha karibuni, kamati ya maji Goba baada ya kukatwa kwa maji ilimwandikia barua mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni tarehe 30/08/2011 yenye kumbukumbu namba G/WP/GOBA/VOL013/11 ikimuarifu Mkurugenzi kuhusu kusitishwa kwa huduma ya Maji kwa Wananchi wa Kata ya Goba.

Katika barua hiyo ambayo mbunge nilipatiwa nakala yake, wananchi hao walimlalamikia mkurugenzi kwa kutozifanya kazi barua zao wakionesha mfano barua ya tarehe 22/05/2011 na kumuomba Mkurugenzi kuchukua hatua za haraka ili huduma ya maji irejeshwe hata hivyo Manispaa ilizembea kuchukua hatua zinazostahili.

Mnamo tarehe 21/03/2011, nilimwandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni yenye namba : KUMB:OMU/MJ/005/2011 yenye kichwa cha barua “Hatua za Haraka zinahitajika kuhusu mradi wa Maji Goba” .

Kutokana na hatua stahili kutochukuliwa niliandika barua nyingine kwa Mkurugenzi yenye kumb. OMU/MJ/008/2011 na kupendekeza hatua za haraka kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha kutoka mfuko wa Jimbo Tsh 3,000,000.00 zinapelekwa haraka katika Akaunti ya maji Goba ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa manispaa za kujenga uwezo wa mradi husika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni alifanya ziara Goba tarehe 31/01/2012 katika ziara ile mkurugenzi aliwaahidi wakazi wa Goba kurejesha huduma ya Maji ndani ya wiki moja lakini hadi sasa ni zaidi ya mwaka wananchi bado hawajapata huduma hiyo.

Tarehe 18/03/2012 niliwaandikia barua tena DAWASA yenye kumbukumbu namba OMU/MJ/006/2012 kuhusu hatua ambazo DAWASA imechukuakuhusu matatizo ya maji katika kata ya Goba, katika barua hiyo nilitaka kujua hatua ambazo DAWASA imechukua kushughulikia matatizo ya maji Goba hususani juu ya kufanya majadiliano na Manispaa ya Kinondoni ili kuwa na mfumo endelevu zaidi wa utoaji wa huduma ya maji katika kata ya Goba ambayo ina ongezeko kubwa la wakazi, makazi na mahitaji mengine mengi kwa sasa.

Wizara ya Maji na mamlaka zingine za kiserikali zinapaswa kuharakisha uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kusababisha uvunjwaji wa haki za watumiaji wa huduma ya maji, udhaifu wa usimamizi wa miradi ya maji na ukosefu wa huduma ya maji katika kata ya Goba kwenye Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam ili kutoa fundisho kwa maeneo mengine.

Kwa kufanya hivyo, Serikali ifuatilie mpaka Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO wawezeshe huduma ya maji kurejea kwa wananchi, kupanua kwa dharura wigo wa upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kata ya Goba pamoja na kuboresha mfumo mzima wa upangaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maji katika Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO.

Aidha ili kupata ufumbuzi wa kudumu Wizara ichukue hatua za ziada ili kata ya Goba itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya Kinondoni na badala yake ihudumiwe na DAWASA pamoja na DAWASCO ili kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu.

Mheshimiwa Spika;
Upungufu katika usimamizi wa Sheria za maji na haja ya kuharakisha utungaji wa kanuni na marekebisho ya sheria husika:

Hatua kuhusu uboreshaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam zinasimamiwa na sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge hili.

Baadhi ya Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji ya mwaka 2009, Sheria ya maji safi na usafi wa mazingira ya mwaka 2009, sheria ya mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji ya mwaka 2001 na sheria ya mamlaka ya maji safi na maji taka Dar es salaam ya mwaka 2001. Hata hivyo kumekuwa na upungufu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo ikiwemo katika kutunga kanuni na kuchukua hatua kwa wakati.

Serikali inapaswa kutoa maelezo bungeni ni kwanini mpaka mwezi Julai mwaka 2012 ilikuwa haijakamilisha kutunga kanuni zinazohusu uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa Maji (National Water Investment Fund) toka Sheria husika itungwe mwaka 2009. Bunge lijadili hoja hii ili pamoja na mambo mengine liisimamie Serikali mfuko huu uweze kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi wote wenye kuhitaji uwekezaji toka mfuko huu kuondoa matatizo ya maji nchini ikiwemo Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika;
Aidha, katika utekelezaji wa sheria umeonekana pia upungufu mwingine wa ziada unaohitaji marekebisho ya sheria mbalimbali. Mfano, ukiondoa maeneo ya mijini ambapo huduma za maji zinasimamiwa na mamlaka za maji safi na maji taka kwa upande wa Dar es salaam ikiwa ni DAWASA; maeneo ya vijijini kote nchini yanayohudumiwa na Halmashauri ikiwemo maeneo ya pembezoni ya Dar es salaam yanayohudumiwa na Manispaa, mifumo ya usimamizi ina udhaifu kutokana na upungufu wa kisheria.

Kutokana na hali hiyo kwa nyakati mbalimbali limetolewa pendekezo na wabunge kwamba paundwe Wakala wa Maji (TANWATER) kama ilivyo Wakala wa Barabara (TANROADS) hata hivyo Serikali mpaka sasa haijatekeleza pendekezo hilo ambalo utekelezaji wake utahusisha pia marekebisho ya sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Spika;
Sheria ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam ya mwaka 2001 nayo inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa. Kati ya mambo yanayohitajika kufanyika ni pamoja na kurekebisha ramani ya awali iliyopitishwa ikiwa ni sehemu ya sheria husika kuhusu eneo ambalo kwa mujibu wa sheria linapaswa kuhudumiwa na DAWASA (designed area) ili kuendana na ukuaji wa jiji pamoja na maeneo jirani ya Kibaha na Bagamoyo.

Aidha, marekebisho mengine yanahitajika katika utaratibu mzima wa DAWASA kutoa mikataba kwa makampuni mengine kuendesha huduma ya maji kwa niaba yake ili kuepusha kasoro zilizojitokeza wakati wa mkataba wa City Water na kasoro nyingine zinazoendelea hivi sasa katika mkataba baina ya DAWASA na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).

Marekebisho yanayohitajika kufanyika ni pamoja na ya kubadili muundo wa Bodi ya DAWASCO ikiwemo kuwezesha uwakilishi wa Halmashauri za Manispaa za Dar es salaam katika bodi ya DAWASA.

Kwa upekee wa muundo wa Mkoa wa Dar es salaam, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inafanya kazi ya uratibu tu wakati ambapo sehemu kubwa ya taratibu za ardhi, mipango miji na ujenzi ziko katika Halmashauri. Halmashauri za Manispaa ndizo ambazo zinahusika kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji ukiondoa ya DAWASA katika kata na mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam.

Hata hivyo, wakati halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inawakilishwa kati bodi ya DAWASA, Manispaa zote tatu hazina uwakilishi hali ambayo inapunguza kiungo cha mawasiliano na kuathiri nguvu za Halmashauri katika kufuatilia miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao na wakati mwingine kuchelewesha miradi husika.

Marekebisho ya sheria ya DAWASA yanapaswa kuhusisha pia kurekebisha adhabu zinazotokana na makosa ya uharibifu wa miundombinu ya maji, wizi wa maji safi na uunganishaji kinyemela wa mabomba ya maji taka; kwa kuwa adhabu zilizopo kiwango chake kimepitwa na wakati na hakilingani na kukithiri kwa makosa ya biashara haramu ya maji na hujuma katika miundombinu ya maji katika jiji la Dar es salaam.

Kasoro katika upangaji na utekelezaji wa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la Maji katika Jiji la Dar es salaam:
Ikumbukwe kuwa katika kutafuta ufumbuzi Mwezi Machi 2011 Baraza la Mawaziri lilipitisha Mpango Maalum wa Maji Dar es salaam na Pwani wenye mgawanyo wa fedha ufuatao:
Mahitaji ya fedha Mpango Maalum

Mahitaji ya fedha Mpango Maalum
Na. Kazi zitakazotekelezwa Gharama
2010-2013
(SH.BILIONI) Makadirio kila mwaka wa fedha (sh. bilioni)
2010/11 2011/12 2012/13 2013/14
1 Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu 17.25 0.45 6.00 6.00 4.80
2 Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini 122.50 9.38 24.28 56.98 31.88
3 Kazi ya visima vya Kimbiji na Mpera 133.15 10.35 70.90 29.25 22.65
4 Ujenzi wa bwawa la Kidunda 174.75 3.00 7.80 83.70 80.25
5 Upanuzi wa mtandao wa mabomba ya maji safi 82.40 - 24.05 37.15 21.20
6 Uchimbaji na ukarabati wa visima katika maeneo yasiyo na maji. 4.00 1.50 2.50 - -
7 Kuimarisha utoaji wa huduma ya maji 18.00 - 5.00 6.00 7.00
8 Kuboresha uondoaji wa majitaka (upanuzi wa mtandao na ujenzi wa mitambo mitatu ya maji taka) 100.60 - - 50.30 50.30
9 Miradi mingine 0.20 0.20 - - -
10 Elimu kwa umma 1.00 0.50 0.20 0.20 0.10

Jumla Kuu 653.85 25.38 140.73 269.58 218.18



Katika kutekeleza mpango huu maalum, natambua kwamba upanuzi wa mfumo wa maji wa Ruvu Juu ikiwemo ujenzi wa wa Tanki la Kibamba na Bomba mpaka Kimara utafanyika na fedha za ujenzi huo kiasi cha dola milioni 132 zimepatikana ikiwa sehemu ya mkopo wa dola milioni 178 kutoka Serikali ya India. Nafahamu pia kwamba ujenzi wa kupanua intake na machujio mapya ya maji unaendelea kwa udhamini wa Shirika la Milenia (MCC) wa kiasi cha dola za kimarekani milioni 36.8. Naelewa pia kuwa ujenzi wa bomba kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam utakaogharimu shilingi bilioni 122.5 za walipa kodi wa Tanzania umeanza.

Hata hivyo, kiwango cha uwekezaji huo hakijaweza kufikisha malengo yaliyopitishwa na Baraza la Mawaziri na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano uliopitishwa na Bunge hili; kwa kuwa jumla mpaka mwaka wa fedha 2012/2013, zilipaswa kuwa zimetumika au walau zimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 435.67 ikiwa ni hatua ya haraka ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na mikoa mingine inayoguswa na miradi hiyo ikiwemo ya Morogoro na Pwani.

Mheshimiwa Spika;
Hivyo, pengo hilo linapaswa kuzibwa kwa haraka kupitia nyongeza ya fedha katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa kuchukua hatua za haraka. Serikali ieleze bungeni imefikia wapi katika kupata fedha za kulipa fidia ya maeneo ya hifadhi ya maji ya Kimbiji na Mpera kiasi cha shilingi bilioni 27 ambayo ilipaswa kuwa imelipwa tangu mwaka 2011 na lini hasa ujenzi utaanza.

Serikali ieleze iwapo ujenzi wa Bwawa la Kidunda Mkoani Morogoro unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 175 utaingizwa katika vipaumbele vya taifa kwa mwaka 2013/2014 kwa kuzingatia umuhimu wa bwawa hilo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yenye kufanya upatikanaji wa maji kutokuwa na uhakika katika mto Ruvu kipindi chote cha mwaka na kusababisha uhaba wa maji kwa wananchi wa Pwani na Dar es Salaam.

Hatua hizi zote zitakuwa na tija kwa wananchi wengi zaidi iwapo zitaambatana na ujenzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika maeneo ambayo hayakufikiwa katika awamu iliyopita; maeneo ambayo wananchi huyaita ‘yaliyorukwa katika uwekezaji wa mabomba ya mchina’ na ukarabati wa mifumo chakavu ya usambazaji wa maji. Serikali inapaswa kueleza ni lini maeneo hayo yatawekewa mtandao wa mabomba ambayo yanakisiwa kuhitaji jumla ya shilingi bilioni 82.4.

Mheshimiwa Spika;
Kwa upande mwingine, ili kuondokana na ‘bomu la wakati’ serikali ione umuhimu wa kutafuta fedha kwa haraka kiasi cha shilingi bilioni 100.6 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji taka kama ilivyoahidi kwa nyakati mbalimbali.

Fedha hizi zinaonekana ni nyingi lakini ni matokeo ya udhaifu wa miaka mingi katika mipango miji katika Jiji la Dar es salaam hali inayosababisha gharama za usambazaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka kuwa kubwa. Upo umuhimu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutambua kwamba ongezeko la zaidi ya asilimia 70 ya maeneo ya makazi ambayo hayajapimwa katika Jiji la Dar es Salaam ikilinganishwa na wastani wa asilimia 30 wa miji mingine mikuu ya mikoa ni hali yenye kuathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi na maisha kwa wananchi kwa ujumla.

Ujenzi wa miundombinu hiyo mipya na ukarabati wa ile chakavu ya usafirishaji hautakuwa na maslahi tu kwa wananchi kwa kuwawezesha kupata huduma bali pia utakuwa na tija kwa nchi kwa kupunguza upotevu wa maji mpaka asilimia 25 na hivyo kudhibiti hasara ambayo inalikumba taifa hivi sasa kutokana na kiwango cha maji kinachopotea kwa Jiji la Dar es Salaam pekee.
Bajeti ndogo ya sekta ya maji na utegemezi wa fedha kutoka nje:

Mheshimiwa Spika;
Fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye sekta ya maji ni kidogo na hata hizo zinazotengwa utegemezi wa wahisani kutoka nje ni mkubwa kwa kiwango cha kuathiri miradi katika Jiji la Dar es salaam na nchi kwa ujumla.

Kujibu wa ripoti ya Hali ya Umaskini na Maendeleo ya Watu mwaka 20112 (PHDR) Fedha za ndani za kutekeleza bajeti ya Sekta ya Maji imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka toka 57% katika mwaka wa fedha 2005/06 hadi 10% kwa mwaka wa fedha 2011/12.

Hali hii imesabababisha kukithiri kwa utegemezi katika vyanzo vya mapato toka nje na kwa wabia wa maendeleo kuwezesha miradi ya maji; fedha ambazo hazipatikani kwa wakati na kwa kiwango kinachokidhi mahitaji.

Kwa mwaka 2011/12 tumeshuhudia kutokutimizwa kwa azimio la serikali la kutenga kiasi cha Dola za Kimarekani 128 milioni kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Maji (WSDP) huku bajeti pangwa ikiwa ni dola za kimarekani 28 milioni tu kwa mwaka huo 2011/12.

Tufahamu kwamba kupungua huku kwa kiwango cha bajeti katika sekta ya maji kunapingana hata na azimio la Sharm el Sheikh la nchi za Umoja wa Afrika la mwaka 2008 la kutaka dhamira na azma ya kuongeza kipaumbele cha kisiasa katika utengwaji na kuwekwa wazi kwa bajeti kwa ajili ya sekta ya maji safi na maji taka.

Mheshimiwa Spika;
Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/2013 umeendelea kuonesha upungufu katika utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo katika sekta ya maji, taarifa zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi sita ya kwanza Jumla ya Shilingi Bilioni 29 tu ndizo zilitolewa ikiwa ni sawa na asilimia 36 katika fedha za ndani. Hali hii ni kidogo ikizingatiwa kiwango kilichoidhinishwa na tume ya mipango kikiwa ni shilingi 48,326,792,184 kwa kipindi cha robo ya kwanza pekee.

Mheshimiwa Spika,
Mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa mipango ya serikali hususani katika ugawaji wa rasilimali fedha ambazo zimeidhinishwa na bunge katika huduma muhimu za jamii kama maji, matokeo yake ni kuwa na huduma mbovu, hivyo napendekeza bunge lijadili hali hiyo na kupitisha hatua za haraka ambazo zitanufaisha nchi kwa ujumla ikiwemo Jiji la Dar es Salaam.

Hatua hizo zitawezesha fedha za miradi ya maendeleo ya maji kutolewa kwa wakati katika miezi iliyobaki ya mwaka wa fedha 2012/2013 na kupewa kipaumbele katika Mpango wa Mwaka wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka 2013/2014.

Mheshimiwa Spika;

Udhaifu katika utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini:

Tangu mwaka 2000 Bunge hili limekuwa likipewa ahadi za utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RWSSP). Wakati maelezo ya kuanza kwa mpango huo yalipoletwa bungeni mwaka 2003, wakati huo ukiitwa mpango wa vijiji kumi (quick wins), yapo maeneo katika Jiji la Dar es salaam ambayo yalikuwa na vijiji na yaliingizwa katika mpango huo. Hata hivyo, mpaka leo miaka takribani kumi baadaye mwaka 2013 maeneo hayo yakiwa yameshapanda hadhi na kuwa mitaa miradi hiyo haijatekelezwa kwa ukamilifu wake.

Maeneo hayo yamekosa maji kwa pande zote, hayajahudumiwa na DAWASA na DAWASCO kwa kuwa yapo kwenye vijiji kumi; na mradi huo wa vijiji kumi haujaweza kuwafanya wananchi hao wapate huduma ya maji.

Hali hii haihusu Halmashauri za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam za Ilala, Kinondoni na Temeke; inahusu halmashauri zote nchini ambazo mpango huo ulipaswa kutekelezwa. Naamini kujadiliwa kwa hoja hii kutawezesha wabunge wenzangu kueleza pia uzoefu katika maeneo yenu ya vijijini na mijini hatimaye kutokana na mapendekezo ya hoja hii; Bunge likapitisha maazimio ambayo yataweza kuchangia katika kurekebisha hali hii.

Mheshimiwa Spika;
Programu hii ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ilipaswa kutekelezwa kwa awamu nne, ambapo utekelezaji wa awamu ya kwanza baada ya kucheleweshwa toka mwaka 2003 ulipaswa kuanza mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011. Kwa maneno rahisi ni kwamba hadi kufikia hivi sasa ilipaswa tayari maji yawe yameshapatikana katika vijiji kumi vya kila halmashauri nchini, hata hivyo ukomo wa muda wa awali ukiwa umeshapita kwa zaidi ya mwaka mmoja; utekelezaji katika maeneo mbalimbali nchini haukufanyika hata robo.

Hali iko hivyo, wakati ambapo fedha zimetumika bila maji kupatikana; katika hatua hiyo ya kwanza jumla ya shilingi bilioni 96.4 zimetumika kwenye “quick wins” hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 2012 huku maji kwa sehemu kubwa kukiwa hakuna; hali ambayo ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Mheshimiwa Spika;
Katika ufuatiliaji wangu kuhusu masuala ya maji katika Manispaa za Jiji la Dar es salaam, katika halmashauri zingine na katika Wizara ya Maji nimebaini kwamba hali hiyo ilisababishwa na mikataba mibovu yenye dalili za ufisadi, kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa makampuni yaliyopewa zabuni katika mazingira ya utata na udhaifu katika mchakato mzima wa zabuni na usimamizi wa miradi.

Matokeo yake watafiti na wachimbaji binafsi wengi wao wakiwa hawana uwezo wa vifaa na wataalamu walipewa kazi na kulipwa fedha bila hata ya mchakato kukamilika; badala ya kuwekwa mfumo wa watafiti kuhusika pia na uchimbaji na kulipwa kwa kadiri na matokeo na hatua iliyofikiwa. Anafanya utafiti mwingine, anachukua fedha zake anakwenda; anayekwenda kufanya uchunguzi ni mwingine naye anachukua fedha zake anakwenda; anayejenga miundombinu ni mwingine, naye anaelekezwa eneo na baadaye kueleza kwamba hakuna maji huku hasara ikiwa imeshapatikana.

Ripoti ya Tathmini (Appraisal Report) ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Rural Water Supply and Sanitation Program) ya mwaka 2010 inaonyesha namna ambavyo awamu ya kwanza katika ya mwaka 2007 mpaka 2010 ilivyoshindwa kutekelezwa kwa ufanisi. Usimamizi wa kutosha wa kibunge unahitajika kuhakikisha awamu ya pili (RSSWP Phase II), ambayo awali ilipangwa ifanyike kuanzia mwaka 2011 mpaka 2014 inafanyika kwa kuanzia na kufanya ukaguzi wa awamu iliyopita.

Bunge lako lijadili hali hii na kupitisha maazimio yenye kuwezesha ukaguzi maalum ufanyike kwenye matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zote nchini ili kasoro hizo zisijirudie katika awamu ya pili ya programu hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika;
Baada ya maelezo hayo sasa naomba kuwasilisha hoja kwa mujibu wa kanuni ya 54 fasili ya (1) (2) na (3) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

MABADILIKO KATIKA HOJA KUHUSU HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM

(Kwa mujibu wa Kanuni 55 (10) ya Kanuni za Kudumu za Bunge)

Kwa kuondoa maneno kuanzia “KWA KUWA, kati ya mwaka 2003….. (yaliyo kuanzia katika ukurasa wa 42 na kuendelea mpaka ukurasa wa 45 yanapoishia maneno maneno)…….. mapendekezo ya mpango wa taifa”

Na kuingiza maneno:

“KWA KUWA, Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini ikiwemo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011 kwa kugharimu dola za kimarekani milioni 292 hata hivyo tathmini ya miaka miwili na nusu ya utekelezaji (mid term review) imebanisha kasoro nyingi katika utekelezaji.

KWA KUWA, Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

NA KWA KUWA, Wizara ya Maji iliandaa waraka maalum wa kuiomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni 653.85 Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa na Baraza la Mawaziri mwezi Machi 2011 lakini utekelezaji wake unaelekea kucheleweshwa mpaka mwaka 2016.

NA KWA KUWA, katika mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/13 Serikali haikutenga kiwango kamili cha fedha kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioidhinishwa na Bunge na kwa kuzingatia mgawanyo wa Mpango Maalum wa Maji Safi na Maji Taka katika Jiji la Dar Es Salaam na kauli ya Serikali ya tarehe 7 Novemba 2012.

NA KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 62 (2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 , Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu.

NA KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 63(3) katika utekelezaji wa madaraka yake bunge laweza kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunga sheria pale utekelezaji unapohitaji kuwapo sheria.

NA KWA KUWA, Malengo ya Kitaifa yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa Mjini maji kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2010 na kwamba malengo hayo kwa Jiji la Dar es Salaam yamesogezwa mbele na kuwekwa malengo mapya ya upatikanaji wa huduma ya maji safi kufikia asilimia 90 na uondoaji wa maji taka kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ichukue hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam:

NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalum wa matumuzi ya fedha matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa.

NA KWAMBA, Kufuatia kauli iliyotolewa bungeni tarehe 7 Novemba 2012 kuhusu Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 Serikali izingatie makisio ya awali ya gharama za mpango huo na kuingiza mahitaji yaliyobaki kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2013/2014 na Bajeti ya mwaka 2013/2014.

NA KWAMBA, Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 29 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kwa dharura katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa ikiwemo iliyozinduliwa Oktoba 2012 yenye kuhitaji miundombinu ya ziada kufikia wananchi zaidi.

NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.

NA KWAMBA, EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali.

NA KWAMBA, EWURA iharakishe kukamilisha mchakato ulioanza wa kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.

NA KWAMBA, Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya mpango wa taifa na bajeti ya nchi.

NA KWAMBA, Serikali iwasilishe bungeni haraka iwezekanavyo muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.”

Naomba kuwasilisha.
…………………

John John Mnyika(Mb)

Jimbo la Uchaguzi-Ubungo